Saturday, November 24, 2012

Fagio la JK lanyemelea tena Makatibu Wakuu


Rais Jakaya Kikwete
Pangua pangua ya Makatibu Wakuu wa wizara na wakurugenzi wa idara mbalimbali, inatarajiwa kufanyika wakati wowote, hali inayozua miongoni mwao kuwa matumbo moto.
Kwa mujibu wa Katiba inayotumika, Makatibu Wakuu wa wizara za serikali wanateuliwa na Rais ambaye kwa sasa ni Jakaya Kikwete.
Chanzo cha habari kimelieleza gazeti hili kwamba fununu za kuwepo mabadiliko hayo zimeanza kuenea kwenye wizara tofauti kwa takribani wiki mbili zilizopita.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, mabadiliko hayo yanatokana na sababu tofauti, ikiwemo baadhi yao kufikia umri wa kustaafu na utendaji duni usioleta ufanisi serikalini.
NIPASHE Jumamosi ilipomtafuta Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi ombeni Sefue, kuelezea suala hilo, simu yake iliita muda wote pasipo kupokelewa.
Lakini ofisa mmoja wa ngazi ya juu katika ofisi ya Waziri Mkuu na ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazeti, alithibitisha kuzisikia taarifa za kuwepo ‘pangua pangua’ ya Makatibu Wakuu.
“Hata sisi tumezisikia hizo taarifa, lakini ninadhani kwa uhakika zaidi watafute wahusika katika ofisi ya Mzee (Rais),” kilieleza chanzo hicho.
Lakini vyanzo vingine vinasema, ofisi nyingi za wizara na idara za serikali kumekuwa na mijadala inayohusu mabadiliko hayo.
Ndani ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wanaozungumzia mabadiliko hayo wanasema, yatakuwa kilelezo cha kutoa mwelekeo wa aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Blandina Nyoni.
“Kama mabadiliko hayo yakifanyika, tutajua mwelekeo wa hatma ya Nyoni,” kinaeleza chanzo kutoka ndani ya wizara hiyo.
Akizungumza na jumuiya ya madaktari waliokuwa kwenye mgomo Februari mwaka, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitangaza kusimamishwa kazi kwa Nyoni na Mganga Mkuu, Dk Deo Mtasiwa.
Pinda alisema kufikiwa kwa hatua hiyo kulitokana na malalamiko yaliyowasilishwa dhidi yao, yakihusu tuhuma mbalimbali.
Alisema zipo tuhuma zikiwemo zilizohusisha sare za wauguzi na vifaa vya kupima virusi vya ukimwi, vilivyonunuliwa vikiwa ni feki na zabuni ya usafi katika Hospitali ya Muhimbili.
Pinda alisema kutokana na malalamiko hayo, ameona ni lazima pawepo na tatizo na kuamua kuwasimamisha ili kupisha vyombo vya dola kuchunguza.
Wakati watendaji hao wizarani wakisimamishwa, Rais Jakaya Kikwete Mei 4, mwaka huu, aliamua kuwatimua kazi waliokuwa Waziri na Naibu Waziri hiyo, Dk. Hadji Mponda na Lucy Nkya.
Dk. Mponda na Dk. Nkya, walitajwa kuwa miongoni mwa waziri wasiofaa kuitumikia serikali, na Rais Kikwete, alipofanya mabadiliko madogo kwenye baraza la mawaziri, hakuwateua tena.
YAHUSISHWA NA UONGOZI ‘MPYA’ CCM
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa hatua ya vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachounda serikali, kuamua kuwashughulikia viongozi na watendaji wabovu, kunaweza kuathiri mabadiliko hayo.
Hivi karibuni, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alitangaza kuwa, chama hicho kitawafuatilia mawaziri na watendaji wa serikali, ili watakaobainika kutokuwa makini, Rais ashauriwe kuwatimua kazi.
Hivyo safu ya watendaji makini wa serikali inahitajika katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ikiaminika kwamba kushindwa kwa serikali iliyopo madarakani kutaigharimu CCM.
Pia inaelezwa kwamba kuwepo kwa watendaji na viongozi ‘wabovu’ kunaweza kusababisha mvutano ama mgogoro kati ya chama tawala na serikali yake, hivyo kutoa mwanya kwa upinzani kupata ushindi mkubwa
.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Design by M.S Chopoti | Bloggerized by Ulimwengu Wa Digital