Tumesikitishwa na habari kwamba Jiji la Mwanza juzi lilikumbwa na vurugu kubwa baada ya askari wa Halmashauri ya jiji hilo kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine wawili wakati askari hao walipokuwa wakijipanga kuendesha operesheni ya kuwahamisha Wamachinga katika eneo walilopewa rasmi na halmashauri hiyo kufanyia biashara.
Polisi waliamua kuingilia kati na kutumia mabomu kuwatawanya Wamachinga hao waliokuwa wamejikusanya kwa ajili ya kuandamana kuelekea katika Ofisi za Jiji kupinga mauaji ya mwenzao.
Lakini katika hali ya kushangaza, Meya wa jiji hilo, Stanslaus Mabula alikana kuitambua operesheni hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na askari wake, akisema Wamachinga hao walikuwa wanafanya shughuli zao kihalali kwa kuwa maeneo hayo walipewa na jiji hilo kufanyia biashara.
Katika kuonyesha utovu wa nidhamu wa askari hao, Meya huyo alisema operesheni hiyo ilikuwa batili, huku akisema kilichofanyika ni uhuni na tayari ameagiza askari wote watatu waliohusika katika tukio hilo wachukuliwe hatua kama wahalifu wengine.
Ni jambo jema kwamba Meya huyo wa Jiji la Mwanza amelichukulia tukio hilo kwa uzito na umakini mkubwa, kwani hadi tunakwenda mitamboni tayari watuhumiwa hao walikuwa wamekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi wakati taratibu zikifanyika ili kuwapeleka mahakamani kujibu tuhuma za mauaji.
Tunasema Meya huyo amefanya vyema kuchukua hatua mapema, kwani tumeshuhudia mara nyingi taasisi mbalimbali zikiasisi mifumo ya kulindana, ambapo huwakingia kifua watumishi wake kila wanapotuhumiwa kuvunja sheria za nchi.
Tunakubaliana naye anapoikana operesheni hiyo iliyoendeshwa na askari hao wahuni wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, kwani hakuna asiyejua kwamba operesheni kama hiyo ikipangwa kufanyika sharti vishirikishwe vyombo vya ulinzi kama Jeshi la Polisi.
Lakini pia tunaambiwa kwamba operesheni hiyo bandia ilifanyika bila Ofisi ya Meya na Mkurugenzi wa Jiji kuwa na taarifa. Hapa ndipo maswali mengi yasiyo na majibu yanapoibuka, hasa pale swali linapoulizwa kuhusu uwajibikaji wa mkuu wa kitengo ambacho askari hao wahuni wanafanya kazi.
Tunasema hivyo kwa kutilia maanani kuwa, haiwezekani askari hao waondoke ofisini wakiwa na silaha za moto kwenda sehemu inayoitwa Miti Mirefu kupambana na Wamachinga na kukwapua bidhaa zao pasipo mamlaka husika kufahamu. Hapa tusisahau kwamba operesheni nyingi dhidi ya Wamachinga katika sehemu nyingi nchini umekuwa mradi wa wakubwa, kwani bidhaa zinazokwapuliwa kutoka kwa Wamachinga hupelekwa kusikojulikana na kuwafaidisha watu fulani.
Tukio hilo la Mwanza liifungue macho Serikali ili itambue dhuluma ambazo mamlaka zake zinawafanyia Wamachinga kwa visingizio mbalimbali. Ni matumaini yetu kwamba Serikali haitajikita tu katika kuwashughulikia askari waliowajeruhi Wamachinga na pia kusababisha kifo cha mwenzao mmoja, bali pia itauwajibisha uongozi wa Halmashauri ya jiji hilo kwa kuzembea kuwasimamia askari wake.MWANANCHI


12:03 AM
Hamed Mazrui


0 comments:
Post a Comment