Siku chache baada ya Madiwani, kumkataa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Fanue Senge, Timu ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji kwa Jamii (SAM), imeibua ubadhilifu wa mamilioni ya fedha za miradi ya sekta ya afya.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa juzi, wilayani hapo mbele, ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Christopher Kangoye, maofisa wa watendaji wa sekta ya afya na wadau wa halmashauri hiyo iliandaliwa na timu hiyo iliyoundwa na wakazi wa wilaya hiyo chini ya Shirika lisilo la Kiserikali la Sikika.
Hata hivyo, timu hiyo ilikutana na upinzani kutoka kwa baadhi ya washiriki, jambo lililomfanya Kangoye ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho kutoa ufafanuzi mara kadhaa ambao ulisababisha kukubaliana na matakwa ya watendaji wa halmashauri hiyo kutaka kupewa muda kujibu hoja hizo kabla ya kupeleka kwa wakazi wengi wa halmashauri hiyo.
Timu hiyo yenye wajumbe 27, 15 ni wawakilishi wananchi na 12 ni wawakilishi wa Sikika, ilitembelea katika vituo vya kutolea huduma ili kujiridhisha na usahihi na uwiano wa taarifa mbalimbali zilizomo katika makabrasha na hali halisi.
Vituo vilivyotembelewa ni Mlembule, Tambi, Godegode, Lumuma, Mnada wa Chisalu, Chitemo, Mima, Igoji, Chaludewa, Chinyika, Chinyanhuku, Chipogolo, Kisima, Gulwe na Mlunduzi, Iyenge, Kibakwe, Mlunga, Wangi, Kidenge, Rudi, Mtamba, Kiboriani, zahanati ya TTC. Maeneo mengine ambayo timu hiyo ilitembelea ni Hospitali ya Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri.
Baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na timu hiyo ambayo pia iliwashirikisha madiwani wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ni ukarabati wa nyumba moja ya watumishi wa sekta ya afya wakati ripoti ya utekelezaji inaonyesha kuwa nyumba nne zimekarabatiwa kwa sh. 5,752,400.
“Kulingana na majibu ya Mganga Mkuu wa Wilaya, timu ilishangazwa kusikia nyumba zilizokarabatiwa kuwa ni tano tofauti na ripoti ya utekelezaji kuwa ni nyumba nne,” alisema Katibu wa Timu hiyo, Richard Msittu na kuongeza kuwa;
“Anashangazwa kwa timu kushindwa kuelewa nini maana ya ukarabati wa aina gani ulifanyika kwani hali halisi inaonyesha ni nyumba moja tu iliyokarabatiwa ambapo zingine ukarabati umehusisha mfumo wa majitaka tu.”
Pia walibaini Halmashauri hiyo ilipanga kufanya matengenezo ya gari katika vituo vya afya Rudi na Kibakwe na kutenga sh. 25,143,428, hata hivyo shughuli iliyoripotiwa kufanyika ni matengenezo ya gari moja namba DFP 5632 ambapo jumla ya sh. 25,103,800 zilitumika.
Aidha, Timu hiyo iligundua kuwepo kwa zahanati zilizokamilika bila kutumika na miaka katika mabano, Wangi (1992), Mlima (2009), Mlunga (2004) na Kiboriani (1996).
Kwa mujibu wa timu hiyo iliyofanyia uchambuzi ripoti za Baraza la Madiwani kwa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa miaka 2010/2011 na 2011/2012, fedha za upanuzi wa stoo ya dawa kutolewa bila kufanya kazi mwaka 2010/2011 na kutoonekana katika bajeti ya mwaka 2011/2012 sh. 10,000,000.
Pia waligundua kukosekana kwa uthibitisho wa mafunzo kutolewa kwa wajumbe 392 wa kamati za usimamizi wa zahanati sh. 8,410,000.
Timu hiyo pia ilibaini kuwepo kwa nyumba za serikali ambazo zinaishi watu wasio watumishi wa serikali huku wanaostahili wakikosa nyumba za kuishi na hivyo kuishi uraiani.
Katika hatua nyingine timu hiyo imebaini halmashauri ilipanga kununua simu tano na vocha kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya na hivyo kutenga sh. 5,700,000 lakini timu hiyo haikupata uthibitisho kuhusiana na kugawiwa kwake.
“Mwaka 2011/12 shughuli iliendelea huku lengo likiwa ni kununua vocha za simu kwa wodi tano ambapo sh 8,772,000 zilikuwepo, sh 6,372,000 ni fedha zilizoidhinishwa na sh 2,400,000 fedha iliyoanzia tofauti na fedha iliyobaki mwaka 2010/11,” alisema Katibu huyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo jumla ya sh 6,875, 000 zilitumika kwa robo tatu za mwaka huku taratibu za manunuzi ya vocha kwa robo ya nne zinaendelea.
“Timu haijapata uthibitisho juu ya uwepo wa simu hizo wodini na kwa mujibu wa majibu ya madodoso hakuna vocha ambazo watumishi walishawahi kupewa kwa matumizi ya ofisi.”
Timu hiyo ilibaini halmashauri hiyo kukiuka kwa kutoa fungu la fedha za kamati za kudumu za Baraza la Madiwani, kamati za masuala ya fedha, afya na elimu.
Jumla ya sh. 3,775,000 zilitumika kulipia posho za vikao vya chama kinyume na kamati zilizokusudiwa kitu ambacho timu iliamini kilichangia kuathiri utendaji kamili wa kamati za kudumu za baraza.
Akizungumza, Mkuu wa shirika la Sikika katika mikoa ya Dodoma na Singida, Patrick Kinemo, alisema timu hiyo imejengewa uwezo na shirika hilo wa kufuatilia uwajibikaji kwa jamii ambao utakuwa ni endelevu.
Alisema katika ufuatiliaji huo waliibua hoja 71 ambazo zinaangukia katika Mpango kabambe wa afya, Ripoti za Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa za Baraza la Madiwani.
Alisema baada ya hoja zilizoibuliwa kupatiwa majibu, wataitisha mkutano wa hadhara ambapo ripoti hiyo iliyoambatanishwa na majibu itawasilishwa kwa wananchi ambao watapata pia nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kangoye alisema kuwa baadhi ya hoja zilizoibuliwa zipo ofisini kwake na kulishukuru shirika hilo kwa kuwajengea uwezo wananchi waweze kufuatilia fedha zinazopelekwa na serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo
.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment