Saturday, November 24, 2012

Membe:Tanzania haitapigana na waasi wa Kongo


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Serikali imekanusha taarifa kuwa itapeleka jeshi lake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kukabiliana na kundi la waasi la M23 , badala yake imesema itapeleka kikosi kimoja cha askari wa miguu kitakachojiunga na jeshi la kimataifa la usimamizi wa amani kulinda mipaka ya nchi hiyo.
Kikosi hicho kitasaidiana na jeshi hilo la amani kulinda mipaka wa DRC na nchi jirani.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alitoa ufafanuzi huo jana kufuatia taarifa zilizochapishwa jana kwenye vyombo vya habari ambazo zinatafsiri kwamba Tanzania inakwenda vitani kupigana na kundi la waasi la M23 nchini DRC.
Waziri Membe alisema kupelekwa kwa kikosi hicho kuna lengo la kulinda mpaka na kudhibiti makundi ya waasi kwa kusaidiana na jeshi la kimataifa ambapo mazungumzo kamili yatafanyika katika mkutano wa kimataifa wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na nchi za SADC.
“Ni bahati mbaya kwamba nilipokuwa naongea na vyombo vya habari jana (juzi) nilinukuliwa vibaya kuwa Tanzania inakwenda DRC kupigana na kundi la waasi la M23, ukweli ni kuwa suala hilo ni kati ya masuala yaliyomo kwenye mapatano ya jeshi la kimataifa la usimamizi wa amani,” alisema.
Aliviomba vyombo vya habari kuwa makini vinapoandika masuala ya vita vya Kongo kwa sababu ni suala linalohitaji uangalifu wa hali ya juu.
Aidha, alisema Rais Jakaya Kikwete atakuwa kati ya wakuu wa nchi waliopangiwa kuhudhuria mkutano huo wa Nchi za Maziwa Makuu na SADC, utakaofanyika jijini Kampala nchini Uganda.
Mkutano huo una lengo la kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la DRC na utaongozwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.
Mkutano huo utakaofanyika leo pia utahudhuriwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa DRC. Joseph Kabila na unatarajiwa kuomba Umoja wa Mataifa (UN) kutokwepa wajibu wao wa kusaidia
 mgogoro wa DRC

.  
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Design by M.S Chopoti | Bloggerized by Ulimwengu Wa Digital