Saturday, November 24, 2012

Mkapa aitaka serikali kusaidia wagonjwa wa figo



Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ameishauri Serikali kupanga utaratibu utakaosaidia wagonjwa wa figo kumudu gharama za matibabu huduma hiyo itakapoanza kutolewa Januari mwakani na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mkapa alitoa ushauri huo jana wakati alipotembelea chuo hicho, kukagua mashine za kisasa 10 za kusafisha damu zilizotolewa na Serikali ya Japan kupitia Mfuko wa Benjamin Mkapa.
Rais huyo msaafu alisema kutokana na uchumi walionao Watanzania wa kawaida hawataweza kumudu kulipia gharama za matibabu hizo kwa kuwa ni ghali sana .
“Gharama za matibabu hayo kwa mtu mmoja kwa mwezi ni zaidi ya shilingi milioni moja na laki mbili sasa kwa mwananchi wa kipato cha chini hawezi kumudu gharama hizi, hivyo Serikali ifikirie kuwasaidia wananchi hawa maana ugonjwa hauchagui tajiri au maskini,” alisema.
Aidha, alisema kwa kuwa hospitali zinazotoa matibabu hayo hapa nchini ni chache hivyo hospitali hiyo ijiandae kuwapokea wangonjwa wengi kutoka ndani ya nchi na nje ya nchi.
Akizungumzia kuhusu msaada wa mashine hizo, Mkapa alisema awali taasisi yake iliomba msaada wa mashine hizo kutoka Japan kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wa Chuo Kikuu hicho ili waweze kujifunza kuwatibu wagonjwa hao.
Hata hivyo, alisema kutokana na mahitaji ya chuo hicho wamebaini ni vema wakaongeza idadi ya wataalam hao.
Naye Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Noah Chihoma, alisema chuo hicho kilipeleka wafanyakazi sita nchini Japan kujifunza jinsi ya kutumia mashine hizo za kisasa za kusafisha damu.
Dk. Chihoma alisema kwa sasa mashine hizo hazijaanza kutumika kwa sababu bado wanasubiri wataalamu wa kutoka kampuni nchini Japan ili waweze kufanya uhakiki wa mwisho ili zianze kutumika.
“Ni kweli tumezipokea mashine hizi kutoka Japan kupitia Mkapa Foundtion na ndio maana tumemwalika Mkuu wa Chuo chetu ambaye ndio aliyetuletea msaada huo ili atuletee wataalam ambao watafanya uhakiki wa mwisho kabla ya kuanza kuzitumia,” alisema.
Alisema pamoja na wataalamu hao sita kutoka hospitali yao, watashirikiana na wataalamu wengine kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuweza kuziendesha mashine hizo.
Dk. Chihoma alisema kwa sasa hospitali yao pamoja na kutibu magonjwa ya kawaida kwa wafanyakazi na wanafunzi, pia inatoa matibabu kwa jamii inayokizunguka chuo hicho.


CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Design by M.S Chopoti | Bloggerized by Ulimwengu Wa Digital