Monday, November 26, 2012

Mwalimu adaiwa kumuua mwanafunzi wake kwa kisu

Mwalimu wa Shule ya Msingi Kwamwachalima iliyopo katika kijiji cha Kwamwachalima, kata ya Komkonga, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Nangoma Suhalungi Nangoma (23), anatuhumiwa kumuua kwa kisu mwanafunzi wake na kumjeruhi mwingine.

Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, polisi wanamtafuta mtuhumiwa huyo ili afikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

Mwalimu huyo anadaiwa kumuua mwanafuzi wa darasa la tatu katika shule hiyo.

Kadhalika, mwalimu huyo anakabiliwa na tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kisaza iliyopo katika kata hiyo.

Habari kutoka katika eneo la tukio ambazo zimethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, zilieleza kwamba tukio hilo lilitokea Novemba 23, mwaka huu saa 9:00 usiku baada ya muuaji kuwavamia watoto hao chumbani kwao na kuwachoma kisu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huku akiwa na huzuni shuleni hapo, baba wa marehemu, Ijumaa Mjaliwa, alimtaja binti yake aliyepoteza maisha kuwa ni Farihia Mjaliwa (9) na aliyejeruhiwa ni Mohamed Mjaliwa (16).

Mohamed ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Sekondari ya Kisaza.

“Aliyemuua mwanangu na kumjeruhi kijana wangu ni Mwalimu mwenzangu ambaye tunafundisha wote hapa shuleni. Alimchoma kisu kifuani eneo la moyoni. Sina ugomvi naye na tunakaa nyumba moja ila usiku mimi sikulala hapa,” alisema Mjaliwa na kuongeza:

“Yeye alikuwa na kesi ya kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili, hivyo alikuwa nje kwa dhamana, jana walimu wote tulifanya kikao cha kujadili namna ya kumuwekea dhamana mahakamani, maana kesho yake kulikuwa na taarifa kwamba angepelekwa mahakamani kujibu mashitaka hayo, ila yeye katika mkutano huo hakuwapo.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo, Ali Hatibu, alisema walimhoji majeruhi huyo kabla hajapoteza fahamu na kumtaja mwalimu huyo kwamba ndiye aliyewachoma kisu pamoja na marehemu.

“Tuliingia chumbani kwa watoto na kukuta damu lakini pia binti huyu ambaye sasa ni marehemu, tulimkuta akiwa tayari amekufa huku akiwa ameshika kisu. Amechomwa kwenye moyo akakiacha mwilini, binti akakichomoa na kupoteza maisha muda huo huo, yaani tukio hili linasikitisha sana maana mtoto hakujua kinachotokea,” alisema Hatibu.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Eva Msenga, alisema siku ya tukio majira ya mchana, alimhoji mwalimu huyo kutokana na mwenendo wake kuonekana si wa kawaida, na kumjibu kwamba amechanganyikiwa kutokana na suala linalomkabili la kufikishwa mahakamani, hivyo alimtaka afike ofisini kwake ajieleze.

“Mimi nilikuwa na watoto hawa usiku hadi saa tatu, wakijisomea nikawaambia wakalale kwa kuwa muda wa kupumzika ulikuwa umefika, wakaenda kulala baadaye usiku wa manane ndipo mtuhumiwa akabisha hodi na kufunguliwa kisha akaanza kufanya ukatili huo wa kutisha,” alidai Msenga.

Akizungumza wakati akiwafariji familia iliyokumbwa na mkasa huo shuleni hapo, Mkuu wa wilaya hiyo Rweyemamu, aliwataka wananchi kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu, akisema kwamba serikali imeanza kumchukulia hatua mwalimu huyo kwa kufunga akaunti yake benki.

Rweyemamu ameomba vyombo vya habari kusaidia kumfichua mtuhumiwa huyo ambaye ni mwenyeji wa mikoa ya Kusini ili sheria ifuate mkondo wake.

“Atakamatwa tu, tutafanya kila namna kwa kuchukua hatua aina zote kuhakikisha kwamba mwalimu huyu anakamatwa ili apambane na mkono wa sheria,” alisema Rweyemamu ambaye alifuatana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Aziz Kimata.

Mwili wa marehemu huyo ulisafirishwa kupelekwa Chalinze wilayani Bagamoyo na mazishi yalitarajiwa kufanyika jana eneo hilo.




 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Design by M.S Chopoti | Bloggerized by Ulimwengu Wa Digital