Monday, November 19, 2012

SASA ISRAELI YAPIGWA VITA MTANDAON

Monday, November 19, 2012



Picha iliyotokea katika tovuti kadhaa za Israeli zilizoripotiwa kudukuliwa na wadukuzi wa kimataifa wa kundi la
Zaidi ya majaribio milioni 44 ya udukuzi yamefanywa kwenye tovuti za Serikali ya Israeli tangu ilipoanzisha mashambulizi ya ndege dhidi ya Ukanda wa Gaza karibu wiki moja iliyopita.

Takwimu zilizotolewa na serikali ya Israeli, zimeonesha kuwa majaribio hayo dhidi ya mitandao inayohusiana na ulinzi yamekuwa ya kiwango cha juu kabisa, huku majaribio milioni 10 yakiwa yamefanywa kwenye tovuti ya rais wa Israeili, milioni 7 kwenye wizara ya mambo ya nje na mashambulizi milioni 3 yamefanywa kwenye mtandao wa waziri mkuu.

Waziri wa fedha wa Israeli, Yuval Steinitz, alisema kuwa jaribio moja tu la udukuzi ndilo lililofanikiwa dhidi ya mtandao ambao hakutaka kuutaja, lakini ulizima na kuendelea kufanya kazi baada ya dakika kumi za kutokufanya kazi.

Anonymous, ambalo ni kundi la kimataifa la harakati za mtandaoni, limeorodhesha tovuti zipatazo 700 za Israeli lilizozishambulia, kuziathiri na kuingilia mawasiliano yake katika kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya ndege yanayoendelea huko Gaza.

Mojawapo ya maeneo muhimu yaliyolengwa katika kampeni hiyo ijulikanayo kama "OpIsrael" ni programu ya maendeleo ya kimataifa iliyo chini ya wizara ya mambo ya nje, Mashav.

Katika tangazo lake kwenye mtandao wa Twitter, kundi hilo la Anonymous lilidai kuwa limeharibu hifadhidata (database) ya ndani ya tovuti hiyo.

Siku ya Alhamisi asubuhi, Anonymous ilitoa taarifa iliyowataka wadukuzi (hackers) wengine kusaidia ku kuharibu na kuzidhuru tovuti zenye mahusiano au zinazomilikiwa na serikali au jeshi la Israeli.

Tovuti ya chama cha Kadima ilivyodukuliwa

Miongoni mwa maeneo muhimu yaliyolengwa ni tovuti ya chama cha Kadima cha Israeli, ambayo ilizimwa baada ya kudukuliwa, na pia tovuti ya Benki ya Jerusalem.

Tovuti nyingi zilizodukuliwa zilionekana kutoweka hewani kabisa, lakini nyingine zilionesha picha na ujumbe uliotoka kwa Wapalestina.
.


Msemaji wa wizara moja ya Israeli alisema kuwa wakati mashambulizi hayo yakiwa yametoka duniani kote, mengi yametoka ndani ya Israeli yenyewe na maeneo ya Palestina.

"Kitengo cha Kompyuta katika wizara kitaendelea kuzuia mamilioni ya mashambulizi ya mtandaoni," alisema Steinitz. "Tunafurahia matunda ya kuweka katika kuendeleza mifumo ya ulinzi ya kikompyuta."

Steinitz ameiagiza wizara yake kushughulika katika mazingira ya dharura ili kukabiliana na mashambulizi yanayozilenga tovuti na mitandao ya serikali.

Pande zote mbili katika mgogoro wa Gaza, hususan Israeli, wanatumia mitandao ya kijamii kama moja ya nyezo zao za vita.

Jeshi la Israeli limekuwa likitumia kila jukwaa, ilhali wapambanaji wa Kipalestina wakitumia zaidi mtandao wa Twitter.

"Vita vinapiganwa katika safu tatu. Safu ya kwanza ni ya ana kwa ana, ya pili ni mitandao ya kijamii duniani na tatu ni udukuzi," hayo yalisemwa na Carmela Avner, afisa habari mkuu wa Israel.

0 comments:

Post a Comment

 
Design by M.S Chopoti | Bloggerized by Ulimwengu Wa Digital