Tangu kianzishwe chuo kikuu cha Dar Es Salaam ambacho ndicho chuo kikuu cha kwanza hapa Tanzania, sasa ni mwaka usiopungua wa 45. Nakumbuka chuo kile ndio chachu ya maendeleo unayoyaona leo Bara kwani vijana kadhaa wenye sifa na wasio sifa waliwezeshwa na kujipatia Elimu yao na wengine magamba yao matupu akina ‘kihio’ na ‘Mulugo’ lakini ndio wanazo digirii zao japo karatasini na sio kichwani. Sisi huku tumeachwa na maneno mengi.
Nakumbuka wazanzibari waliowakipata nafasi ya kujiunga pale kwa mwaka ilikuwa ni watu kumi kama sikosei. Sasa wewe fikiria chuo kikuu kizima kinachukuwa Wazanzibari kumi tu hadi mwishoni mwa miaka ya 1990. Na hata baada ya hapo idadi ya Wazanzibari katika chuo hicho kikuu na vyengine vya bara hairidhishi. Na hii haikutokana na kuwa kulikuwa hakuna wenye sifa huku Zanzibar. La hasha! Ndio muundo wetu wa Muungano. ‘Wanyime Elimu, tuwatawale’
Kuanzishwa kwa Chuo kikuu cha Taifa- SUZA, Chukwani na Tunguu, kumemkombowa na kumfunguwa macho Mzanzibari kwa kiasi kikubwa. Naamini kitendo hiki hakikuwaridhisha watawala wetu kwani sisi kama koloni lao hatuna haki ya kusoma elimu ya juu, kwani tutajuwa kudai haki zetu na usawa. Na hili haliepukiki. Tumesoma, japo hivyo hivyo kimazabe mazabe, na sasa tunahoji Muungano na hata usawa katika nyadhifa mbali mbali ndani ya Muungano. Hili pia haliwapendezi wenzetu.
Hata hivyo,moja kati ya vikwazo vikubwa ambavyo kwa sasa vinawakabili wanafunzi wa Zanzibar kusonga mbele Elimu ya juu hasa kiwango cha Masters na PhD ni ukosefu wa Udhamini. Naamini kuna ‘scholarship’ lukuki zinazokuja Tanzania, lakini zote hazitufiki sisi huku Zanzibar. Na hata hizo chache zinazoletwa wakubwa zetu huzifungia mabweta kwani huwa hawana mtoto wao, mjomba wala shangazi yao mwenye sifa, kwa hio hata wenye sifa wakiwepo, wote nao wakose. Hivi ndivyo tulivyo.
Kule Bara mwaka jana Chevening Scholarship, hakuna Mzanzibar aliepata. Ndio tunajuwa kuna udini katika Scholarship na hili halina shaka hata Chembe. Kuna Common wealth Scholarship kule, sisi hatupati dumu dawamu, kuna usiasa huko dhidi ya Wazanzibari. Kuna Scholarship zikiletwa hapa na kumfikia Bwana Ameir Njeketu. Ukiritimba mtupu na majibu ya kupuuzi na hata akizitangaza bado siku mbili ‘deadline’, hatupati. Ndio sisi kwa sisi hao!
Scholarship pekee ambazo Mzanzibari hupata nadra sana ni za ubalozi wa Marekani, nazo basi zisipitie Zanzibar na pia ni kwa juhudi na heshima ya wawakilishi wa ubalozi wa Marekani waliopo Zanzibar. Hizi kuna vijana wetu wanaozipata lakini ni ‘haba nasi’ kusema kweli. Na kwa mantiki na sababu kama hizi utakuta bado Wazanzibari hatuendi usoni katika Elimu ya juu. Kuna wazanzibar lukuki hivi sasa hapa Nyumbani wenye
‘Admission’ za vyuo mbalimbali lakini wameshindwa na udhamini. Hawana msaada.
Muungu haachi mjawe. Muda mfupi uliopita tumeenda Tunguu kushuhudia uzinduzi wa ‘Scholarship’ za Sultan Qabus wa Oman kwa chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA). Scholarship hizi hazina lolote isipokuwa neema na mafanikio tele kwa Wazanzibar iwapo lengo lilokusudiwa litasimamiwa kwa misingi ya haki, ukweli na uwazi. Udhamini huu wa Elimu ya juu kutoka Oman utawadhamini Wazanzibar 5o kila mwaka kwenda kusoma katika ngazi tafauti katika vyuo tafauti tafauti duniani.
Kheri iliyoje hii kutoka kwa muumba. Kwa sasa akina sisi wenye watoto wa kusoma, tumeingia tamaa kupita mpaka kwani kama watakwenda vijana 50 kila mwaka baada ya miaka kumi tutakuwa na wangapi? Haya ni mafanikio makubwa. Hongera sana mfalame Qabus, sadakatu jaariya yako hii baba!Mungu akuzidishie kheri na sie tuneemeke zaidi wakitaka watawala wetu.
Lakini wakati tukijipongeza na kufurahia neema hii najihisi macho yana machozi na moyo unanipiga kwa kasi kwa woga. Hii ni ishara ya kuwa nina wasiwasi. Khofu yangu kubwa ni kuwa jee, Udhamini huu utamnufaisha Mzanzibar kweli? Siamini na sitaki kuamini kama msaada huu utamnufaisha Mzanzibari, ispokuwa tutarajie moja kati ya matatu yafuatayo kwa udhamini huu.
Kwanza, iwapo Udhamini huu utasimamiwa kwa haki wakapatiwa kweli Wazanzibari watupu 50 kila mwaka, udhamini huu hautafika miaka mine utakufa. Wenzetu wa bara watauchochachocha mpaka ukatike uondolewe. Na hili si geni kwao kutufanyia. Tulikuwa na maonyesho ya Biashara hapa wakati wa Komando Salmin. Waliyapiga vita mpaka yakasimama na kufa kabisa. Wao hadi leo wana sabasaba wala hatuwahoji. Na hili hawataliacha lifanikiwe. Tuombe uhai.
Pili,Ikiwa watashindwa kulifanya hili la kwanza kuanzia sasa watapandikizwa vijana wa bara zaidi ya elfu hapa wengi wao waliofeli la saba, kidato cha nne na cha sita ‘mapyoro’, na wenye digirii za akina ‘Vihio’ na ‘Mulugo’, wakishakuja watapewa vitambulisho na vyeti vya kuzaliwa vya Zanzibar. Wasijaofanyiwa tohara watafanyiwa hapa usiku usiku. Wasiovaa buibui na hijabu watajifunza hapa hapa mpaka wafanane na sisi. Hawa ndio watakaopata nafasi hizi za mfalme Kabusi na sisi tutabaki kusema ‘nami nilipeleka maombi’, au tutaambiwa hatujui ‘kimombo’ kama vile akina ‘Mulugo’ ndio wanaojua kusema hicho kiluga cha wazungu zaidi kuliko sisi.
Tatu, nafasi hizi zitatolewa na wanasiasa ama Wizara ya Elimu Shamuhuna na wenzake, ama Afisi ya makamo wa pili wa Rais, ama Ofisi kuu ya CCM kisiwa ndui. Haya sasa niambie kuna mzanzibari atakaepata nafasi ya masomo hapo? Unamjuwa nani atakwenda kusoma hapo? Wataitana wabara kama walivyokuja hapa akina Zakia Meghji, Seif Ali Idd, Sefu Bakari, Jumbe, Mwinyi, na wengineo wengi waliokuja hapa na kuchukuwa vyeo vyetu chini ya mwavuli wa Uzanzibari. Walipokwisha kufanikisha yao hapana mmoja aliepo sasa. Jumbe yuko mji mwema Kigamboni. Mwinyi kwake Msasani sijui Sitabei, Meghji kwao Bara, Sefu Idd hajamaliza kazi yake tu. Wakimaliza wote hujua kwao hawa. Hawajifichi.
Kwa sasa nabakisha shaka zangu hizo tatu tu lakini naamini kwa nguvu yote hivi ndivyo ‘Scholarship’ za Qabus zitakavyotolewa na zitakavyosimamiwa. Wazanzibari wachache mno watakaonufaika na hizi na kama hatuamini tukae mkao wa kula. Kila la heri na ‘Scholarship’ za Qabus.
Zanzibar ni njema, atakae aje!
NA MZALENDO


1:45 AM
Hamed Mazrui


0 comments:
Post a Comment