Askari watatu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia ya Swetu Fundikira wamewasilisha nia ya kukata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji Zainabu Mruke.
Wakili wa wanajeshi hao Mluge Kaloli aliwasilisha mahamakani nia ya kukata rufaa jana, akieleza kuwa hukumu iliyotolewa dhidi ya wateja wake haikuwa ya haki.
Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni MTM 1900 Sajenti Rhoda Robart (42) wa JKT Mbweni, MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa JKT Kunduchi na MT 85067 Koplo Mohammed Ally wa JKT Mbweni.
Wakili huyo ameeleza sababu ya kukata rufaa kwamba ni ushahidi kwamba kulikuwa na ugomvi kati ya marehemu na wanajeshi hao na kwamba kulikuwa hakuna kusudio la kuua kwani halipo katika sheria ya makosa ya jinai.
“Hakuna shahidi aliyeithibitishia mahakama kwamba washtakiwa walimuua Swetu Fundikila na wajibu wa kuthibitisha kosa si la washtakiwa bali ni la upande wa mashtaka,” alidai.
Kaloli alisema anaiomba Mahakama ya Rufaa kuangalia upya ushahidi uliotolewa kwani mashahidi wote wanamtaja Swetu Fundikira kuwa ni mshtakiwa wakati daktari katika ripoti yake anamtaja marehemu kuwa ni Swetu Abdallah Fundikira.
“Mashahidi wote waliofika mahakamani hakuna hata mmoja aliyeweza kuieleza mahakama kwamba alifika na kushiriki katika maziko ya marehemu,” alidai.
Mapema Novemba 20, mwaka huu Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam iliwahukumu askari hao kunyongwa hadi kufa baada ya ushahidi wa mazingira kuwatia hatiani
.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment