Wednesday, December 12, 2012

Wanahabari watakiwa kuandika habari zinazowahusu walemavu wa akili


Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria Chuo kikuu cha Zanzibar Tunguu Ali Uki amesema Wanahabari wanajukumu la kuzipa kipaumbele habari zinazohusu Watu wenye Ulemavu wa Akili katika vyombo vya habari ili kubadilisha mtazamo hasi wa jamii juu ya Walemavu hao.
Uki ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa Mada ya Wajibu wa Wanahabari kuandika taarifa kuhusu Walemavu wa akili katika Warsha ya siku mbili iliyofanyika ukumbi wa Eacrotanal mjini Zanzíbar.

Amesema kuzipa kipaumbele habari zinazowahusu walemavu zitaifanya jamii kuwaangalia walemavu wa Akili kwa jicho la huruma na kuona kuwa matatizo yao yanaigusa jamii kama ilivyokuwa kwa watu wasio na ulemavu.
Amewaomba wanahabari hao kujikita katika kuandika habari zinazohusu maendeleo ya Walemavu badala ya kuandika habari zinazowakashifu au kudhalilisha hadhi yao.
Akizungumzia kuhusu kesi zinazowahusu walemavu waliofanyiwa udhalilishaji Uki amewataka wanahabari kufuatilia mwenendo wa kesi hizo ili kujua hatima zake kama wanavyofanya kwa kesi za viongozi wa kisiasa.
Kwa upande wake Mjumbe wa Jumuiya kwa ajili ya Watu wenye ulemavu Khalid Omar amesema familia zinawajibu wa kutoa matunzo kwa watu wenye Ulemavu wa Akili ikiwemo kupatiwa haki sawa ya chakula,mavazi na malazi kama watu wengine wasio na ulemavu.
Aidha ameiomba jamii kufahamu haki na usawa wao katika sheria sambamba na kuwajumuisha Walemavu hao katika shughuli zao bila kuwafanyia ubaguzi wa aina yoyote.
Ametoa wito kwa Serikali na Jumuiya za kiraia kuungana pamoja katika kuzitetea na kuzilinda haki za Wenye ulemavu wa Akili ili waweze kuishi na kufanya kazi sambamba na watu wasio na ulemavu katika nyanja zote za maisha.
Jumuiya kwa ajili ya Watu wenye ulemavu wa akili Zanzíbar (ZAPDD) yenye wanachama 1989 ilianzishwa mwaka 1999 ambapo malengo yake makuu ni kupigania haki za watu wenye ulemavu wa akili zikiwemo Elimu,Afya na Ulindwaji ili wathaminiwe kama watu wengine.
 
Imetolewa na Maelezo Zanzibar

0 comments:

Post a Comment

 
Design by M.S Chopoti | Bloggerized by Ulimwengu Wa Digital